Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa taarifa kwa umma na walipakodi wote kuhusu hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo mpya wa kisasa wa usimamizi wa kodi za ndani unaojulikana kama Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumo wa IDRAS umeunganishwa na mifumo ya taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa, kuongeza uwazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa walipakodi na wadau wengine. Mfumo huu unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Januari 2026.
TRA imeeleza kuwa IDRAS itamwezesha mlipakodi kujihudumia mwenyewe (self-service) popote alipo na wakati wowote, kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), jambo litakalorahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za kikodi.
Huduma Zitakazotolewa Kupitia IDRAS
Mfumo wa IDRAS unakwenda kuchukua nafasi ya mifumo yote ya sasa ya usimamizi wa kodi za ndani. Baadhi ya huduma zitakazopatikana kupitia mfumo huo ni pamoja na:
- Usajili wa walipakodi
- Uwasilishaji wa ritani za kodi
- Ulipaji wa kodi
- Uwasilishaji wa mapingamizi na rufaa za kodi
- Marejesho ya kodi
- Misamaha na vivutio vya kodi
- Usajili wa mashine na utoaji wa risiti za kielektroniki
- Maombi ya hati ya ulipaji kodi (Tax Clearance)
- Utoaji wa leseni mbalimbali
Mafunzo ya Matumizi ya Mfumo wa IDRAS
Ili kuwajengea uelewa walipakodi na wadau kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa IDRAS, TRA imetangaza kuanza kutoa elimu na mafunzo maalum kwa umma. Mafunzo hayo yataanza tarehe 17 Desemba 2025 saa kumi jioni, na yatafanyika kwa njia ya mtandao (virtual).
TRA imewahimiza walipakodi wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kujifunza namna ya kupata na kutumia huduma zitakazotolewa kupitia mfumo wa IDRAS mara utakapozinduliwa rasmi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni