Wagombea 33 kutoka vyama vya siasa 17 wanagombea nafasi ya Ubunge na Udiwani katika uchaguzi mdogo unaofanyika leo kwenye baadhi ya maeneo nchini.
Kati ya wagombea 33, wagombea 21 sawa na asilimia 63.64 ni Wanaume na wagombea 12 sawa na asilimia 36.36 ni Wanawake.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, amesema uchaguzi huo mdogo unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo.
Aidha, uchaguzi wa ubunge unafanyika katika jimbo la Siha lililopo Mkoani Kilimanjaro, na Jimbo la Fuoni lililopo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, visiwani Zanzibar.
Pia, kata tano za Tanzania Bara zinafanya uchaguzi huo am,bazo ni Pamoja na kata ya Chamwino iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mbagala Kuu iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, na Nyakasungwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa, Mkoa wa Mwanza.
Kata nyingine ni Masoko iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, na kata ya Ndono iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, jumla ya Wapiga Kura 218,024 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanashiriki katika uchaguzi huo na jumla ya vituo 556 vya kupigia kura vinatumika.
Aidha, mawakala wametakiwa kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni