Afisa Mkaguzi wa Ndani Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Bw. Hamis Mjanja, amewataka Wakuu wa Vitengo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kuweka mikakati madhubuti ya kusimamia na kulinda mali za umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs), ili kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kwa tija na kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza leo Desemba 16, 2025 Jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Vitengo wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Bw. Mjanja amesema kuwa usimamizi dhaifu wa rasilimali umekuwa chanzo cha upotevu wa rasilimali hizo hususan rasilimali fedha, hali inayokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema Sekretarieti za Mikoa zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwepo na mifumo thabiti ya usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwemo kuimarisha udhibiti wa ndani, ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali na uwajibikaji wa watendaji.
“Ni wajibu wa Wakuu wa sehemu na Vitengo ngazi ya Mkoa kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na nidhamu ya fedha, ili kuzuia aina yoyote ya uhalibifu na ubadhilifu wa Mali za Umma” amesema Bw. Mjanja.
Aidha, amewasisitiza Wakuu wa Vitengo kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza ipasavyo maamuzi ya Serikali kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo inayosimamia utendaji kazi katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mkagunzi wa Ndani Mkuu ameeleza kuwa usimamizi bora wa rasilimali za umma unapaswa kwenda sambamba na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, akibainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, kwa ubora unaokubalika na kwa gharama stahiki.
Mafunzo hayo ya uongozi yamelenga kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo katika masuala ya uongozi, usimamizi wa rasilimali za umma na uwajibikaji, ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni