Breaking

Jumatatu, 15 Desemba 2025

WANANCHI MOROGORO NA KILIMANJARO WANUFAIKA NA HUDUMA MPYA ZA MAWASILIANO


Kampuni ya mawasiliano ya Airtel imezindua minara mitatu mipya ya mawasiliano katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro, hatua inayolenga kuboresha huduma za mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.


Minara hiyo imejengwa wilayani Gairo, Kata ya Magoweko, Kihonda VETA kijiji cha Yespa mkoani Morogoro pamoja na Kata ya Sanya Juu mkoani Kilimanjaro. Ujenzi wa minara hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mtandao wa simu na intaneti katika maeneo yaliyokuwa na changamoto ya mawasiliano.


Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja wa Airtel Kanda ya Kilimanjaro, Faustine Mtui, alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kupanua wigo wa huduma bora na za uhakika kwa wananchi wote nchini.


Mtui alisema tayari zaidi ya vijana mia tatu wilayani Gairo wananufaika na ajira za uwakala wa Airtel, na kuongeza kuwa uwepo wa minara hiyo utaongeza ajira, kuboresha huduma za kifedha na kukuza shughuli za kibiashara.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Magoweko, Shabani Sajilo, alisema kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakikumbana na changamoto ya kukosa mtandao wa kuaminika, hali iliyokuwa ikiathiri biashara, mawasiliano ya dharura na shughuli nyingine za maendeleo.

Hakuna maoni: