Breaking

Jumatatu, 15 Desemba 2025

WATANZANIA WAMEOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOMO YA UZAMILI SWEDEN

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden umetoa wito kwa Watanzania kuchangamkia maombi ya fursa za masomo ya uzamili kwa mwaka 2026/27 nchini Sweden kwa udhamini wa Taasisi ya Sweden (SI) ili Tanzania ipate nafasi zaidi.


Akitoa taarifa hiyo, Balozi Mobhare Matinyi alisema kwamba baada ya kikao na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Kimataifa ya SI, Kurt Bratteby, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Programu ya Ufadhili wa Masomo na Uongozi, Bi. Adiam Tedros, mnamo tarehe 29 Oktoba, 2025, walimweleza kwamba kwa mwaka wa masomo wa 2025/26 Tanzania ilipata nafasi 11 tu.


Bi. Tedros alisema Tanzania ni moja ya mataifa yanayotuma maombi machache ya wanafunzi kila mwaka na hivyo kusababisha nchi ipate nafasi chache kulinganisha na mataifa mengine ambayo hupata nafasi hadi 40.


Katika kikao hicho Balozi Matinyi aliuomba uongozi wa Sl utoe kipaumbele zaidi kwa Watanzania wenye sifa watakaoomba watakaoomba mara hii akiahidi kwamba Ubalozi utahakikisha Watanzania wengi wanapata taarifa za fursa hizi na kutuma maombi.


Fursa za ufadhili kwa mwaka huu zimejikita katika maeneo ya taaluma za utawala, afya ya umma, ujasiriamali na ubunifu, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati. Mwombaji anatakiwa kwanza kuomba nafasi kwenye chuo kikuu kupitia tovuti rasmi ya 

https://www.universityadmissions.se/intl/start kufikia tarehe 15 Januari, 2026.


Baada ya kupata udahili, mwombaji atatakiwa kuomba ufadhili kupitia tovuti 

https://si.se/en/apply/scholarships/swedish-institute-scholarships-for-global-professionals/ kufikia tarehe 26 Februari, 2026.


Watanzania watakaohitaji maelezo zaidi wanashauriwa kuwasiliana na Ubalozi kupitia barua pepe: mail.box@tanemb.se.


Imetolewa na:


Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Sweden 15 Desemba, 2025.

Hakuna maoni: