Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa jitihada zake za kuendelea kuboresha sekta ya usafiri majini nchini.
Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo, leo tarehe 15 Desemba 2025, alipotembelea Banda la TASAC katika maonesho yaliyoambatana na Mkutano wa 18 wa Tathmini wa Sekta ya Uchukuzi, yanayoendelea katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kitaifa jijini Arusha.
Akizungumza bandani hapo Mhe. Kihenzile ameipongeza TASAC kwa juhudi za kusimamia sekta ya usafiri majini ikiwa ni pamoja kusimamia vituo vya utafutaji na uokoaji ili kupunguza ajali zinazotokana na vyombo vya usafiri majini.
"Hongereni kwa kuendelea kusimamia sekta ya usafiri majini na udhibiti wa bandari. Ukuaji wa bandari hasa bandari ya Bagamoyo utasaidia kuongezeka kwa kasi ya uingizaji wa kiwango kikubwa cha mizigo nchini na kupelekea kuongezeka kwa pato la taifa,” amesema Mhe. Kihenzile.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohammed Salum ameelezea kuwa majukumu ya TASAC ni kusimamia na kudhibiti usafiri majini kwa kuzingatia kuboresha huduma za usafirishaji majini, kuboresha usalama wa usafiri majini, usalama na ulinzi na utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa pamoja na huduma za biashara za meli.“TASAC imeendelea kuhakikisha inasimamia suala la usalama katika bahari na maziwa makuu kwa kutumia boti za uokoaji lakini pia boti ya matibabu yenye vifaa vya kitabibu ambayo inatumika kuhudumia watakaookolewa pale itatokea ajali majini", amesema Bw. Salum.
TASAC inashiriki Mkutano wa 18 wa Tathmini wa Sekta ya Uchukuzi ulioanza tarehe 15 Desemba 2025 na unatarajiwa kufikia kilele tarehe 17 Desemba 2025.
Mkutano huu unawakutanisha wadau kutoka sekta ya usafiri nchini ambapo hutumia jukwaa hili kufanya Tathimini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni