Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ashatu Kijaji amesema tuzo za utalii Duniani (World Travel Awards 2025) ambazo Tanzania imejizolea ni matokeo chanya ya jitihada mahsusi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour, ambayo imeitangaza Tanzania kimataifa.
Akizungumza jijini Dodoma Desemba 15, 2025 mara baada ya kupokea rasmi tuzo ambazo Tanzania ilishinda katika hafla ya kimataifa iliyofanyika Desemba 6, 2025 nchini Bahrain, Dkt.Kijaji amesema kuwa tukio hilo ni fursa ya kutafakari mafanikio ya Sekta ya Utalii na kutambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia.
Amesema kupitia juhudi hizo Dunia imeona utajiri wa urithi adhimu wa Maliasili, Utamaduni, amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa na muungano kwa ujumla.
“Kupitia Royal Tour, dunia imejionea kwa macho yake utajiri wa vivutio vyetu vya asili, malikale, utamaduni na uwekezaji wa utalii,"amesema Dkt. Kijaji.
Ameongeza kuwa, jitihada hiyo imeimarisha kwa kiasi kikubwa taswira ya Tanzania kama nchi salama, yenye amani na vivutio vya kipekee, hali iliyopelekea ongezeko la watalii, kuongezeka kwa imani ya wawekezaji, pamoja na kuipa Tanzania ushindani mkubwa katika soko la utalii duniani
Pamoja na kuzishukuru sekta binafsi kwa mchango mkubwa wa upatikanaji wa tuzo hizo ameahidi kuwa Wizara anayoingoza itaendelea kushirikiana na sekta hizo pamoja na kuendelea na dhamira thabiti ya kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wa utalii.
Katika Tuzo hizo, Tanzania imeibuka na tuzo ya World’s Leading National Park – Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, World’s Leading Balloon Ride Operator – Serengeti Balloon Safaris, World’s Leading Exclusive Private Island – Jumeirah Thanda Island , Africa’s Best Corporate Retreat Destination – Zanzibar.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni