Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kusimamia vyema miradi 15 katika
Pori la Akiba Mpanga Kipengere ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na jamii ianze kunufaika na matunda ya uhifadhi wa rasilimali za Maliasili.
Mhe. Kijaji amesema hayo alipotembelea katika Pori hilo ikiwa ni mwendelezo wa kutembelea shughuli za Uhifadhi na vivutio vya Utalii vilivyopo hapa nchini, amesisitiza TAWA kutumia vyema fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubora na kiwango cha juu ikionesha uhalisia wa fedha zilizowekezwa.
"Hapa kuna miradi 15 iliyowekezwa katika kipindi hiki kifupi cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, niwatake TAWA kuweza kuisimamia kwa umakini miradi hii, iweze kudumu ili tuweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ya uwepo wa miradi hii katika eneo letu, ili tuweze kuenzi kazi nzuri iliyofanywa na Rais wetu, ili thamani halisi ya fedha iweze kuonekana na wananchi waone matunda ya sh.billion 4.14 zilizowekezwa" amesema Mhe. Dkt.Kijaji
Aidha, Mhe. Kijaji ameilekeza Mamlaka hiyo kuangalia fursa mpya za uwekezaji zilizopo kwenye eneo hilo na kuzitangaza ili kuendelea kuongeza wageni kutoka ndani na nje ya nchi na hatimaye kufikia malengo ya serikali ya watalii Milioni 8 ifikapo mwaka 2030.
"Tuwaite wawekezaji, tuwauzie fursa wawekeze nasi li watanzania na wasio watanzania wanaofika hapa Mpanga Kipengere waweze kulala na kula kwa amani kabisa, hivyo kaeni na mtoke na maandiko ya kuuza fursa tulizonazo kama alivyofungua mipaka Rais wetu kupitia Filamu ya Royal Tour" amesema Mhe. Kijaji.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Hamad Hassan Chande , ametoa wito kwa Mamlaka hiyo kuendelea kuimarisha ushirikiano kati yao na jamii katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa ili ziendelee kuwa na tija kwa kizazi hiki na kijacho ikiwa ni zao la asili
"Endeleeni kuimarisha mahusiano yenu, wanajamii mmekuwa walinzi wazuri wa rasilimali zetu. Niwasihi endeleeni kuiishi vyema falsafa ya kazi na utu, hivyo niwaombe wanakijiji tuendelee kuhifadhi na kuzilinda rasilimali zetu kwa wivu mkubwa sana kwa sababu hii ni neema aliyotupa Mwenyezi Mungu" amesema Mhe. Chande









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni