Ufanisi wa Bandari ya Zanzibar umetajwa kuongezeka katika siku za karibuni baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga Scanner mpya ya kisasa ya kukagua makontena yanayoingia bandarini hapo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamishna Mkuu wa (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda alitembelea bandarini hapo tarehe 17.12.2025 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Bw. Akif Ali Khamis amesema kabla ya kufungwa kwa Scanner hiyo walikuwa wakitumia saa tatu mpaka tano kukagua kontena moja lakini hivi sasa wanatumia saa moja kukagua kontena 100.
Amesema kuongezeka kwa kasi ya kukagua makontena kumeongeza idadi ya mizigo inayopita bandarini hapo kwa siku pamoja na mapato ya bandari kwa ujumla hali ambayo imewavutia watu wengi zaidi kupitisha mizigo yao katika Bandari hiyo.
"Kuongezeka kwa mizigo kwenye Bandari yetu kumeongeza mapato ya bandarini sambamba na makusanyo ya Kodi, Tunaishukuru sana TRA kwa kufunga Scanner kwenye Bandari yetu ya Zanzibar" amesema Bw. Khamis.
Kwa upande wake Kamishina Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kufungwa kwa Scanner hiyo kumeongeza usalama wa nchi kufuatia ukaguzi unaofanyika ambao unaonyesha kila kilichomo kwenye kontena na kuzuia vihatarishi.
Amesema kupitia Scanner hiyo ya kisasa wamewezesha biashara kufanyika kwa urahisi kufuatia kuongezeka kwa idadi ya mizigo inayopita bandarini hapo ambayo pia itaongeza makusanyo ya kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA imekuwa ikifanya kila jitihada kuongeza wigo wa kodi, kwa kuwezesha biashara na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni