Breaking


Jumamosi, 24 Januari 2026

MAHAKAMA YAMPUNGUZIA PRESHA RAMADAN SOBHI, KIFUNGO CHA JELA KUSITISHWA


 Hatma ya kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Misri, Ramadan Sobhi, imechukua mwelekeo mpya baada ya Mahakama kukubali rufaa yake dhidi ya hukumu ya kifungo cha miaka mitatu jela aliyokuwa amepewa awali katika kesi ya kughushi.


Kwa mujibu wa taarifa rasmi za kisheria, Mahakama imeamua kusitisha utekelezaji wa adhabu hiyo, hatua inayompa Sobhi afueni kubwa huku mchakato wa kisheria ukiendelea. Awali, nyota huyo wa soka alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia katika kesi iliyomhusisha na tuhuma za kughushi nyaraka, jambo lililozua mjadala mpana ndani na nje ya Misri.


Uamuzi huo wa Mahakama umekuja kama pigo kwa upande wa mashtaka, lakini ni faraja kubwa kwa mchezaji huyo ambaye amekuwa akisisitiza kutokuwa na hatia tangu mwanzo wa kesi. Kupitia mawakili wake, Sobhi aliwasilisha rufaa akieleza kuwa hukumu ya awali ilikuwa na mapungufu ya kisheria pamoja na ushahidi usioridhisha.


Kwa sasa, kusitishwa kwa kifungo kunamaanisha kuwa Ramadan Sobhi hatarejea jela, angalau hadi uamuzi wa mwisho utakapofikiwa. Hatua hiyo pia inampa nafasi ya kuendelea na majukumu yake ya kisoka bila vikwazo vya kifungo, ingawa suala hilo bado linaendelea kufuatiliwa kwa karibu na mamlaka husika.


Kwa mashabiki wa soka barani Afrika, hasa wale wa Misri, taarifa hii imepokelewa kwa hisia mseto wapo wanaoona ni ushindi wa haki, huku wengine wakisubiri kwa hamu kuona hatima ya mwisho ya kesi hiyo.


Ramadan Sobhi ni mmoja wa wachezaji waliowahi kung’ara katika klabu za Ulaya na Afrika, na sakata hili la kisheria limekuwa kivuli kikubwa katika taaluma yake. Uamuzi wa Mahakama kukubali rufaa yake sasa unafungua ukurasa mpya, huku macho yote yakielekezwa kwenye hatua zinazofuata za kesi hiyo.


Hakuna maoni: