Breaking


Jumatatu, 19 Januari 2026

Msiba Hispania: Ajali ya Treni za Mwendo Kasi Yaua Watu 21, Makumi Wajeruhiwa

 



Takribani watu 21 wamepoteza maisha kufuatia ajali mbaya ya treni za mwendokasi iliyotokea kusini mwa Hispania, huku mamlaka za nchi hiyo zikionya kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka kadri juhudi za uokoaji na matibabu zinavyoendelea.

Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi wa Hispania, Oscar Puente, zaidi ya watu 30 wanapatiwa matibabu ya majeraha makubwa hospitalini, huku jumla ya watu 73 wakiripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.

Ajali hiyo ilitokea karibu na mji wa Adamuz, eneo lililo karibu na jiji la Cordoba, wakati treni ya mwendokasi iliyokuwa ikisafiri kutoka Malaga kuelekea Madrid ilipoacha reli na kuvuka hadi kwenye njia nyingine, kwa mujibu wa taarifa kutoka Adif, mwendeshaji wa mtandao wa reli nchini humo.


Baada ya kuacha reli, treni hiyo iligongana na treni nyingine iliyokuwa ikitokea Madrid kuelekea Huelva, na kusababisha madhara makubwa pamoja na taharuki kwa abiria waliokuwamo ndani ya treni zote mbili.


Huduma za dharura za eneo la Andalusia zilieleza kuwa tukio hilo lilihitaji operesheni kubwa ya uokoaji kutokana na ukubwa wa ajali na idadi ya waathirika.


Waziri Puente alielezea tukio hilo kuwa “la ajabu sana”, akibainisha kuwa reli ambayo treni iliacha ilikuwa imetengenezwa upya Mei mwaka jana, jambo linalozua maswali mengi kuhusu chanzo halisi cha ajali hiyo.


Hadi sasa, chanzo rasmi cha ajali bado hakijafahamika, huku ikielezwa kuwa uchunguzi wa kina kubaini kilichotokea utachukua takribani mwezi mmoja.


Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, alisema taifa hilo linakabiliwa na “usiku wa maumivu makali”, akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao.


Kampuni binafsi ya reli Iryo, iliyoendesha treni iliyokuwa ikisafiri kutoka Malaga, ilithibitisha kuwa takribani abiria 300 walikuwamo ndani ya treni hiyo, huku treni nyingine inayoendeshwa na shirika la Renfe ikiwa na karibu abiria 100.


Uchunguzi unaendelea huku taifa hilo likiomboleza msiba mkubwa uliotikisa sekta ya usafiri wa reli nchini Hispania.


Hakuna maoni: