Breaking


Jumatatu, 19 Januari 2026

SIMBA WA TERANGA WAANDIKA HISTORIA: SENEGAL YATWAA UBINGWA WA AFCON 2025 BAADA YA KUICHINJA MOROCCO

 


Timu ya Taifa ya Senegal, maarufu kama Lions of Teranga au Simba wa Teranga, imeandika historia mpya katika soka la Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika fainali kali iliyochezwa usiku wa Januari 18, 2026 nchini Morocco.

Fainali hiyo iliwakutanisha wababe wawili wa soka barani Afrika, huku Senegal na Morocco zikionesha kiwango cha juu cha ushindani, nidhamu ya kiufundi pamoja na mapambano makali yaliyojaa tahadhari na umakini mkubwa kutoka kwa wachezaji wa pande zote mbili.


Dakika 90 za kawaida za mchezo huo ziliisha bila mshindi, kutokana na uimara wa safu za ulinzi na ubora wa makipa wa timu zote mbili, hali iliyolazimu kuchezwa kwa dakika 30 za muda wa nyongeza ili kumpata mshindi wa taji hilo kubwa barani Afrika.

Hatimaye, dakika ya 107 ya mchezo, mashabiki wa Senegal walilipuka kwa furaha baada ya mshambuliaji Pape Alassane Gueye kufunga bao la pekee na la ushindi, bao lililodumu hadi filimbi ya mwisho na kuipa Senegal ubingwa wao wa pili wa AFCON katika historia ya mashindano hayo.


Kwa mafanikio hayo, Senegal imejinyakulia zawadi ya Dola za Kimarekani Milioni 10, sawa na takribani Shilingi Bilioni 24.7 za Kitanzania, ikiwa ni ongezeko kubwa la fedha za zawadi ikilinganishwa na michuano ya AFCON 2023. Hatua hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inalenga kuongeza ushindani, motisha na hadhi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.


Kwa upande wao, wenyeji Morocco waliomaliza nafasi ya pili wamepokea zawadi ya Dola za Kimarekani Milioni 4, kama ilivyotangazwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa CAF wa kuzipa motisha timu zinazofika hatua za juu za mashindano.


Matokeo hayo yanaifanya Morocco kupoteza fainali ya pili ya AFCON katika historia yao, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo mwaka 2004 walipopoteza dhidi ya Tunisia.


Kwa ushindi huo, Senegal inazidi kujiimarisha kama moja ya mataifa makubwa ya soka barani Afrika, ikithibitisha uimara, uthabiti na ubora wake katika anga la soka la Afrika.


Hakuna maoni: