Breaking


Jumapili, 11 Januari 2026

MWANZA YAZIDI KUNG’ARA KUPITIA MIRADI YA UMWAGILIAJI

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inaendea kuinua hadhi ya Mkoa wa Mwanza, kupitia utekelezaji wa Miradi ya Umwagiliaji kutokana na wananchi kuanza kunufaika na ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mahiga. 

Mradi huo umetajwa kuwa  umeleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kilimo.Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Davidi Silinde, mkoani humo. 

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi 12 ya Umwagiliaji inayotekelezwa mkoani humo, ambapo minne inafanya kazi kikamilifu na mingine minane ipo katika hatua za ukarabati. 

Silinde amesema kuwa mabonde 43 yameainishwa kuwa na uwezo wa kilimo cha Umwagiliaji na kwamba miradi mitatu ya sekta binafsi imeonesha mchango wa wadau katika kuendeleza sekta hii muhimu. 

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesisitiza wakulima waache kutegemea kilimo cha msimu kinachotegemea mvua pekee na badala yake kujikita katika kilimo cha Umwagiliaji. 

Kwa mujibu wa Silinde, miradi ya ukarabati imekuwa chachu ya mageuzi makubwa ambapo Skimu ya Katunguru yenye hekari 3,750 imefikia asilimia 90 ya utekelezaji na inatarajiwa kukamilika Mei 2026. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba,  Ng’walabuza Ludigija ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa inazozifanya kuhakikisha wakulima wanapata fursa ya kulima kwa tija, kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wao pamoja na upatikanaji wa chakula cha kutosha. 

Naye  Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Mwanza amesema mradi wa skimu ya Umwagiliaji ya Mahiga unatekelezwa kwa viwango vya juu vya kitaalamu, ukiwa umejumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo mifereji mikuu miwili yenye urefu wa jumla ya mita 5,500, mifereji ya shambani, barabara za mashambani zenye urefu wa mita 5,000, vigawa maji, birika la kunyweshea mifugo na kuongeza kimo cha tuta la bwawa, yote yakilenga kuhakikisha maji yanawafikia wakulima kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Hakuna maoni: