Juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimeiwezesha Sekta za utalii na wanyamapori kuendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa pato la Taifa, kuleta ajira kwa mamilioni ya Watanzania, pamoja na kulinda rasilimali zilizorithishwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Jijini Dodoma kwenye kikao chake na Wadau wa sekta za Utalii na Wanyamapori chenye lengo la kujadiliana kwa uwazi, kubadilishana uzoefu na kuweka mwelekeo wa mustakabali wa sekta hizo.
Dkt. Kijaji amesema kuwa ni wazi maendeleo ya sekta hizo hayawezi kufikiwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa kweli na wa kudumu kati ya Serikali, Sekta Binafsi, asasi za kiraia, wawekezaji na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Amesisitiza kuwa hali ya utalii nchini kwa sasa iko imara na inaendelea kuimarika, kwa takwimu za kuanzia mwezi Januari hadi Novemba mwaka 2025, idadi ya Watalii imeongezeka kwa asilimia 9.02 kufikia watali 2,097,823 ikilinganishwa na Watalii 1,924,240 kipindi kama hicho kwa mwaka 2024 ikiakisi pia ongezeko la mapato yanayotokana na utalii.
"Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwezi Oktoba, mapato yatokanayo na utalii yamefikia Dola za Kimarekani bilioni 4.2, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi yetu, huku idadi ya watalii ikiendelea kuongezeka kwa kasi". Alisema Dkt. Kijaji
Pamoja na kuwapongeza Wadau hao, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi makini wa Jemedari wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta za utalii na wanyamapori kwa lengo la kupunguza gharama kwa wawekezaji, kurahisisha taratibu na kuongeza ushindani wa Tanzania kimataifa.
"Mageuzi haya yamejumuisha marekebisho ya tozo na ada pamoja na kuboresha mifumo ya kiutendaji". Amesema Dkt. Kijaji
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amemuhahidi Dkt. Kijaji kuwa ofisi yake itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau kwa maendeleo endelevu ya sekta ya Utalii na Wanyamapori.
Kikao hicho kimeudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Nkoba Mabula, Wakuu wa Idara, Vitengo na wa taasisi za Wizara hiyo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni