Breaking


Jumatatu, 5 Januari 2026

SERIKALI YAAINISHA ORODHA YA BIDHAA NA HUDUMA MIGODINI AMBAZO HAZIPASWI KUFANYWA NA WAGENI

 

WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde,ametangaza rasmi orodha ya huduma na bidhaa 20 zinazopaswa kutolewa migodini kupitia kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 ikiwa ni hatua ya uhakikisha fedha zinazotokana na shughuli za madini zinabaki ndani ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 5, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Mavunde amesema hatua hiyo inalenga kupanua ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa sekta ya madini, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za madini.

Amesema utekelezaji wa hatua hiyo umefanyika baada ya kufanyika marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za Mwaka 2018, hatua iliyotoa nafasi zaidi kwa kampuni za kitanzania kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini.

Ameeleza kuwa, kwa awamu ya kwanza, Tarehe 14 Novemba 2025, Tume ya Madini ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania, ambapo kwa mara ya kwanza tangazo hilo lilifanyika kupitia Kanuni ya 13A.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, matokeo ya utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania yameanza kuonekana, ambapo manunuzi ya huduma na bidhaa kutoka kampuni za kitanzania yameongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.85 sawa na asilimia 62 ya manunuzi yote ya Shilingi trilioni 3.01 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 sawa na asilimia 88 ya manunuzi ya Shilingi trilioni 5.00 yaliyofanyika mwaka 2024.

Kwa upande wa ajira, amesema idadi ya Watanzania wanaofanya kazi katika miradi ya madini imeongezeka kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024, hali inayoonesha kuimarika kwa nafasi za ajira kwa wazawa.

Ameongeza kuwa, katika nafasi zinazohitaji utaalamu wa juu unaohusisha teknolojia za kisasa, Serikali imeweka utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania ili kuchukua nafasi zinazoshikiliwa na wataalamu wa kigeni, akitolea mfano Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold), ambapo nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania kwa asilimia 100.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde amesema Serikali inaendelea kupanua wigo wa ushiriki wa Watanzania kwa kutenga eneo maalum la uwekezaji katika eneo la aliyekuwa Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi lenye ukubwa wa ekari 1,331 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zitumikazo migodini, ambapo tayari viwanda sita vimejengwa na wawekezaji 15 wameonesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo

Hakuna maoni: