Breaking


Jumanne, 6 Januari 2026

SUPER EAGLES WANG’ARA AFCON 2025, WAICHAPA MSUMBJIJI 4-0 NA KUTINGA ROBO FAINALI

 

Nigeria imejihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Fes.


Super Eagles walionyesha ubora wao tangu dakika za mwanzo wa mchezo, wakitawala umiliki wa mpira na kuandaa mashambulizi ya hatari. Ndani ya dakika mbili za mwanzo, mshambuliaji nyota Victor Osimhen alifanikiwa kutikisa nyavu, lakini bao lake likafutwa kwa sababu ya kuotea.


Shinikizo la Nigeria liliendelea hadi dakika ya 20, ambapo Ademola Lookman alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti la kiufundi, akimalizia pasi ya kurudishwa nyuma kutoka kwa Akor Adams. Dakika tano baadaye, Osimhen aliongeza bao la pili baada ya mpira uliopigwa na Lookman kugonga Adams kabla ya kumkuta Osimhen aliyekuwa tayari kuutumbukiza wavuni.


Msumbiji, iliyokuwa ikishiriki hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yake ya AFCON, ilionekana kulemewa na kasi, nguvu na uzoefu wa Nigeria, ikishindwa kuunda nafasi hatarishi mbele ya lango la wapinzani wao.


Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile, Osimhen akifunga bao lake la pili binafsi na la tatu kwa Nigeria, akimalizia pasi safi ya Lookman iliyopita kutoka upande wa kushoto hadi nguzo ya pili. Mshambuliaji Akor Adams alihitimisha karamu ya mabao dakika ya 75 kwa bao la nne, baada ya tena Lookman kuonyesha ubunifu na mchango mkubwa katika ushindi huo.


Nigeria, ambayo ingeweza kuongeza mabao zaidi kutokana na nafasi walizotengeneza, sasa inasubiri mshindi kati ya Algeria au DR Congo katika robo fainali itakayopigwa Jumamosi mjini Marrakech, kuanzia saa 16:00 kwa saa za GMT. Ushindi huu unaendelea kuionyesha Nigeria kama moja ya timu tishio katika mbio za kutwaa ubingwa wa AFCON 2025.


Hakuna maoni: