Venezuela imeingia kwenye kipindi kigumu cha taharuki ya kisiasa na kiusalama baada ya Rais Nicolás Maduro kutangaza hali ya dharura katika eneo lote la taifa hilo. Hatua hiyo imekuja kufuatia mashambulizi ya Jumamosi yaliyodaiwa kufanywa na Marekani, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serikali ya Caracas.
Katika tamko lake, serikali ya Venezuela imeeleza kuwa uamuzi wa kutangaza hali ya dharura ni hatua ya dhahiri ya kulinda uhuru wa kisiasa na rasilimali za taifa. Rais Maduro amesisitiza kuwa nchi hiyo haitakubali kuingiliwa wala kuporwa rasilimali zake muhimu.
Rais huyo pia ameliagiza jeshi la taifa kutekeleza kwa ukamilifu mipango yote ya ulinzi “kwa wakati unaofaa na katika hali zinazofaa,” huku akizitaka taasisi zote za kijamii na kisiasa kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha na kuhamasisha wananchi. Serikali imeyataja mashambulizi hayo kuwa ni ya kikolonialisti, ikidai yana lengo la kuidhoofisha Venezuela kisiasa na kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi yaliyodaiwa kufanywa na Marekani yalilenga rasilimali za kimkakati, hususan mafuta na madini, sambamba na juhudi za kuharibu uhuru wa kisiasa wa taifa hilo la Amerika Kusini.
Tangazo la hali ya dharura linaongeza mzigo wa changamoto ambazo Venezuela imekuwa ikikabiliana nazo kwa muda mrefu, ikiwemo mashinikizo ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Wachambuzi wanaonya kuwa hatua hii inaweza kuwa na athari kwa maisha ya raia wa kawaida pamoja na mwelekeo wa uchumi wa ndani endapo hali itaendelea kuwa tete.
Kadri macho ya dunia yanavyoelekezwa Venezuela, bado haijabainika hali hii ya dharura itaendelea kwa muda gani na itachukua mwelekeo upi katika uhusiano wa kimataifa wa nchi hiyo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni