Breaking


Jumamosi, 31 Januari 2026

WAZIRI MKUU ATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumamosi, Januari 31, 2026 ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha utalii.

Waziri Mkuu amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuviuza vivutio vyetu vya utalii duniani kote, sote ni mashahidi namna alivyoshiriki filamu za Tanzania The Royal Tour na The Amazing Tanzania ambazo zimechochea kuitangaza Tanzania na vivutio vyetu kimataifa.”

“…Na ndiyo maana na mimi nimepata msukumo wa leo kuja hapa kujionea vivutio vyenu kama sehemu ya kumuunga mkono kwa jitihada zake hizo.”

Akiwa katika hifadhi hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake za uhifadhi kuendelea kutunza mazingira ya hifadhi mbalimbali nchini ili ziwe endelevu.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili wafaidi uzuri wa nchi yao, kwani vivutio hivyo havipo kwa watalii wa kigeni pekee.

Pia, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na mazingira ya hifadhi hiyo ukiwemo uoto wa asili, ambapo amesisitiza wananchi nao washiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

“Ukiona uoto huu wa asili unaoonekana hapa, inaonesha dhahiri namna Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TANAPA walivyofanya kazi nzuri ya kuutunza uoto huu.”

“Tutunze rasilimali ili ziwe na faida hadi kwa vizazi vijavyo. Mmeona maji safi yanayotiririka hapa, tumeelezwa hayaishii humu hifadhini, wakazi walioko nje ya hifadhi hii wananufaika nayo pakubwa.”

Amesema ameelezwa kuwa bei ya kutembelea hifadhi hiyo kwa mtalii wa ndani ni shilingi 11,000 tu, ambayo anaamini Watanzania wengi wanaweza kuimudu, hivyo wajiwekee ratiba ya kuitembelea.

“Tuwe na utaratibu kama wenzetu, wao wanapofunga safari kuja kutembelea vivutio wanajiandaa kwa kuanza kutenga fedha mwaka mzima, kila mwezi anatenga fungu kwa ajili ya kwenda kutalii.”

Pamoja na mambo mengine akiwa hifadhini humo, Waziri Mkuu ameshuhudia uwepo wa mti mkubwa aina ya Mkuyu wenye miaka zaidi ya 100 pamoja na maporomoko ya maji ya Tululusya.

Vivutio vingine vinavyopatikana hifadhini humo ni ndege aina ya flamingo, wanyamapori kama mbega, nyati, twiga, pundamilia, kima wa bluu (blue monkeys), na pia ukiwa ndani unaweza kuona vilele viwili vya Mlima Meru pamoja na kuupanda. Aidha, kuna matembezi ya miguu (walking safari) ambayo humpa mtalii fursa ya kukaribia vivutio.

Pia kuna utalii wa usiku (night game drive) unaomwezesha mtalii kuona wanyama ambao mchana hawaonekani wakiwemo chui, fisi na muhanga. Kadhalika, alitembelea kuona utalii wa kitamaduni kwenye jamii zinazozunguka hifadhi.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu aliongozana na mkewe Mama Neema Mwigulu.

Hakuna maoni: