Breaking


Jumatatu, 16 Februari 2026

ANGALIZO: VIPINDI VIFUPI VYA MVUA KUBWA KUTARAJIWA KATIKA BAADHI YA MIKOA

 


Mamlaka ya hali ya hewa imetoa utabiri wa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo, Februari 16, 2026, ikitoa taarifa ya uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi. Mikoa inayotarajiwa kupata mvua hizo ni pamoja na Dodoma, Morogoro, Rukwa, Iringa, Njombe, Songwe, Mbeya na Ruvuma, ambapo wakazi wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.


Kwa mujibu wa utabiri huo, mikoa ya Dodoma na Singida inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu, mvua na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo pamoja na vipindi vifupi vya jua. Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika mikoa ya Morogoro, Mtwara na Lindi, huku mvua zikinyesha kwa maeneo machache na kuambatana na radi.


Kwa upande wa nyanda za juu kusini ambazo ni Rukwa, Ruvuma, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe, kunatarajiwa hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo kadhaa, huku baadhi ya maeneo yakishuhudia vipindi vifupi vya jua. Katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi, hali ya hewa inatarajiwa kuwa ya mawingu kiasi, mvua na radi katika maeneo machache.


Kaskazini mwa nchi, mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache pamoja na vipindi vya jua. Kwa upande wa ukanda wa pwani, ikiwa ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam na Pwani (ikiwemo Mafia), hali ya mawingu, mvua na ngurumo za radi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo. Vilevile katika visiwa vya Unguja na Pemba, kunatarajiwa hali ya mawingu na mvua katika maeneo machache.


Kwa ukanda wa Ziwa Victoria unaojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu, hali ya mawingu, mvua na radi inatarajiwa katika baadhi ya maeneo hasa nyakati za mchana na jioni.


Aidha, viwango vya joto, mawio na machweo ya jua kwa baadhi ya miji hapa nchini vitatofautiana kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea. Wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa rasmi zaidi na kuchukua tahadhari hususan katika maeneo yatakayopata mvua kubwa kwa vipindi vifupi.


Hakuna maoni: