Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Dhamana (CMSA) kuendelea kutoa elimu ya masuala ya uwekezaji kwa wanachi ili waweze kuwekeza kwa faida.
Mhe. Balozi Omar, alitoa maagizo hayo wakati wa kikao chake na uongozi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Dhamana (CMSA) kilichofanyika Ofisi za Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Alisistiza kuwa elimu ya uwekezaji ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia Watanzania kuelewa fursa zilizopo na namna ya kuzitumia kwa manufaa ya kiuchumi.
“uwekezaji sahihi kupitia masoko ya mitaji unachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa” Alisema Mhe. Balozi Omar.
Aliipongeza Mamlaka ya CMSA kwa ukuaji wa thamani ya uwekezaji kwa asilimia 128 ambapo kwa mwaka 2021 kulikuwa na ukuaji wa shilingi trilioni 28 na hivi sasa ukuaji huo umefikia shilingi trilioni 65.2.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Dhamana (CMSA), Bw. Lucas Mwimo, alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa Bodi yake itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.
Alisema kuwa, Bodi ya CMSA inatambua umuhimu wa elimu ya uwekezaji na itaongeza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ya kukuza uchumi wa wananchi.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama, alisema kuwa wamepiga hatua kubwa katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye masoko ya mitaji.
“Tulikuwa tunaendelea na zoezi la kutoa elimu na kampeni za uhamasishaji ambalo limechangia ongezeko la washiriki wapya, ambapo Watanzania wengi sasa wanajitokeza kuwekeza kwa njia rasmi na salama”, alifafanua Bw. Mkama.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade na Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionisia Mjema.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni