Breaking


Jumamosi, 21 Februari 2026

WIZARA YA AFYA YAONGEZA MSUKUMO WA MAWASILIANO YA CHANJO NCHINI

 

Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga na Mpango wa Taifa wa Chanjo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na wadau wa sekta ya afya, inaendelea kuimarisha utoaji na uhamasishaji wa huduma za chanjo nchini kwa lengo la kuongeza msukumo wa matumizi ya chanjo kwa maslahi ya jamii.


Hayo yameelezwa na Afisa Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau, Februari 20, 2026 jijini Arusha, wakati wa kikao kazi cha kukamilisha rasimu ya Mkakati wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma kuhusu Huduma za Chanjo.


Bi. Gadau amesema mkakati huo una mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi, kuondoa hofu na mashaka, na kuhamasisha matumizi sahihi ya huduma za chanjo. Amefafanua kuwa kupitia vyombo vya habari, mikutano ya kijamii na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs), mkakati huo utasaidia kujenga imani kwa mfumo wa afya na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia.


“Mkakati wa mawasiliano utawawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu aina na umuhimu wa chanjo, na kupunguza upotoshaji unaotokana na uvumi au imani potofu,” amesema.


Ameongeza kuwa Wizara ya Afya ina jukumu la kutunga sera, miongozo na mikakati ya kuboresha huduma za chanjo, kuratibu Mpango wa Taifa wa Chanjo, kufuatilia usalama wa chanjo (AEFI) na kujenga uwezo wa watoa huduma katika mawasiliano rafiki kwa jamii.


Naye Msimamizi wa Chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Rosalia Arope, amesema TAMISEMI ni kiungo muhimu kati ya sera za kitaifa na utekelezaji wake katika ngazi za mikoa na halmashauri. Amesema taasisi hiyo inaratibu utekelezaji wa huduma za chanjo, kuhamasisha viongozi wa mitaa na kuwezesha mikutano ya kijamii ili kuhakikisha mkakati wa mawasiliano unawafikia wananchi moja kwa moja.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mabadiliko ya Tabia za Kijamii kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumba, amesema UNICEF inaendelea kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu katika programu ya chanjo, kuendeleza mikakati ya mawasiliano inayolenga jamii (SBCC na RCCE) pamoja na kufanya tafiti za kubaini sababu zinazochangia baadhi ya wananchi kusita au kukataa chanjo.


Hakuna maoni: