Breaking


Jumatano, 4 Februari 2026

DKT. KIJAJI: UWEKEZAJI UTALII UZINGATIE MASLAHI YA TAIFA NA WANANCHI KWANZA

 



Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amewataka viongozi na wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini yake kuzingatia uzalendo, sheria na maslahi mapana ya Taifa kabla ya kusaini mikataba yoyote ya uwekezaji katika sekta za uhifadhi na utalii, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na rasilimali za Taifa.


Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na wataalam kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kilicholenga kumpa uelewa wa kina kuhusu kanuni, sheria na mifumo ya uwekezaji katika sekta ya utalii na uhifadhi. Amesisitiza kuwa mikataba yote ya uwekezaji inapaswa kuzingatia kwanza manufaa ya Taifa badala ya maslahi binafsi.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Waziri amesema katika uongozi wake atasimamia kwa dhati maslahi ya wananchi na maendeleo ya Taifa, huku akibainisha kuwa hakutakuwa na nafasi ya upendeleo au maslahi binafsi katika usimamizi na uendelezaji wa maliasili za nchi.

Aidha, Dkt. Kijaji ameelekeza maeneo yote yaliyopewa wawekezaji yasimamiwe ipasavyo na kuendelezwa kwa wakati kwa mujibu wa sheria na mikataba husika, ili kufikia matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha rasilimali za Taifa zinaacha tabasamu kwa Watanzania kupitia ajira, mapato na maendeleo ya kijamii.


Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Kijaji amekutana na wasimamizi wa Fedha za Maendeleo ya Utalii Tanzania (TDL) kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji wa mfuko huo na mchango wake katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu Bw. Nkoba Mabula pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo.


Hakuna maoni: