Breaking


Jumatano, 4 Februari 2026

SERIKALI YAIPONGEZA VODACOM KWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA UCHUMI WA KIDIGITALI NCHINI

 


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa sekta ya mawasiliano katika kukuza uchumi jumuishi wa Taifa, hususan kupitia mageuzi ya uchumi wa kidigitali, ulipaji kodi na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Mhe. Balozi Omar aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. David Tarimo, katika Ofisi za Hazina Treasury Square, jijini Dodoma. Katika kikao hicho, Waziri huyo alieleza kuwa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano yamekuwa nguzo muhimu katika kuharakisha ukuaji wa uchumi na kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.

Akizungumza zaidi, Waziri wa Fedha aliishauri sekta ya mawasiliano nchini kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni. Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa yana mchango mkubwa katika kuongeza ukwasi kwa makundi mbalimbali ya jamii, hususan vijana, na kuchochea ubunifu pamoja na ajira katika uchumi wa kidigitali.


Mhe. Balozi Omar pia aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuvutia mitaji zaidi katika sekta ya mawasiliano. Alibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza mchango wa sekta hiyo katika kuboresha maisha ya wananchi, huku ikiwawezesha wawekezaji kupata faida endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Tanzania, Bw. David Tarimo, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini. Alisema kuwa mazingira hayo yameiwezesha sekta ya mawasiliano kuchangia kodi ya zaidi ya shilingi trilioni 1.1 katika mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo Vodacom pekee imechangia zaidi ya shilingi bilioni 621 hadi kufikia mwezi Machi, 2025.


Aidha, Bw. Tarimo alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Vodacom Tanzania, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 4.5 katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano nchini. Aliongeza kuwa katika mwaka 2025 pekee, Vodacom ilitoa msaada wa zaidi ya shilingi bilioni 3.7 kwa jamii kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali katika sekta za afya, elimu, mazingira pamoja na kuwawezesha vijana kiuchumi.

Kikao hicho muhimu pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, Mkurugenzi wa Masuala ya Nje wa Vodacom Tanzania, Bi. Zuweina Farah, pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Kampuni ya Vodacom.


Hakuna maoni: