Breaking


Alhamisi, 5 Februari 2026

ENG. SAMAMBA: KILA SIKU NI FURSA MPYA KUISUKUMA TANZANIA KUWA KITOVU CHA UONGEZAJI THAMANI WA MADINI AFRIKA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amesema kila siku ni fursa mpya kwa Tanzania kujiimarisha katika ajenda ya uongezaji thamani wa madini na kujenga nafasi yake kama kitovu cha uongezaji thamani wa madini barani Afrika.

Eng. Samamba ametoa kauli hiyo leo, Februari 5, 2026, katika ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mtumba, wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo waliompongeza kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Ameeleza kuwa mshikamano na umoja unaooneshwa na watumishi ni msingi muhimu wa kufanikisha malengo ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini, soko linalokua pamoja na mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo ni jukumu la kila mdau wa sekta ya madini kutumia fursa hizo kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi, kukuza ajira kwa Watanzania na kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha, Eng. Samamba amebainisha kuwa Wizara ya Madini itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sekta, kuhamasisha uwekezaji katika teknolojia za kisasa za uchakataji wa madini, pamoja na kusukuma mbele utekelezaji wa Madini Vision 2030  “Madini ni Maisha na Utajiri”, kwa lengo la kuifanya sekta ya madini kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda na uchumi jumuishi nchini.

Akisisitiza dhamira hiyo, Eng. Samamba amesema:

“Sote tuliopo hapa tumebarikiwa kwa uwepo, afya na uzima. Kila siku ni nafasi ya kufanya zaidi kutimiza lengo la uwepo wetu hapa duniani. Kwa sisi tuliopo katika Sekta ya Madini, kila siku ni fursa ya kuisukuma sekta hii kufikia malengo ya kitaifa. Mwelekeo wa sasa ni kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi, kuuza bidhaa za mwisho, kujenga uwezo na kuharakisha maendeleo kwa Taifa, jamii na vizazi vijavyo.”

Kauli hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi, viwanda na ustawi wa Watanzania kwa ujumla.

Hakuna maoni: