Msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop na anayefahamika kama King of Trap Music, T.I (Tip Harris), ameweka wazi mipango yake ya kustaafu rasmi kufanya muziki wa Rap baada ya kuachia albamu yake ya mwisho inayotarajiwa kutoka mwaka huu.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, T.I amesema amefika wakati wa kufunga ukurasa mmoja muhimu wa maisha yake ya muziki na kuanza safari mpya nje ya studio na jukwaa la muziki. Msanii huyo ameeleza kuwa Mungu amembariki kwa vipaji vingi zaidi ya muziki, na sasa angependa kuvitumia kwa kina akiwa karibu na familia yake, watoto na wajukuu zake.
“Mungu amenibariki kwa uwezo mwingi. Nimefanya muziki kwa muda mrefu, sasa nataka kutumia muda wangu kufanya mambo mengine muhimu nikiwa na familia yangu,” amesema T.I.
T.I amebainisha kuwa kustaafu kwake hakumaanishi mwisho wa ubunifu au mchango wake katika jamii, bali ni fursa ya kuwekeza zaidi kwenye biashara, uigizaji, ujasiriamali na majukumu ya kifamilia ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakisubiri nafasi.
Hii si mara ya kwanza kwa rapa huyo mwenye historia ndefu kwenye tasnia kuzungumzia suala la kustaafu. Mwaka 2023, T.I aliwahi kueleza kuwa baada ya zaidi ya miaka 20 kwenye muziki, anahisi ameshafanya mengi na hana uhakika kama ataendelea kuwa kwenye game kwa muda mrefu zaidi kama ilivyokuwa awali.
Katika safari yake ya muziki, T.I ameacha alama kubwa kupitia albamu na nyimbo zilizotamba duniani kama “Whatever You Like,” “Live Your Life,” “Rubber Band Man,” “24’s” na nyingine nyingi zilizoleta mapinduzi kwenye muziki wa Trap na Hip Hop kwa ujumla.
Tangazo lake limezua hisia mseto kwa mashabiki wake, ambapo wengi wameonyesha mshangao, huzuni na shukrani kwa mchango wake mkubwa katika muziki wa Rap duniani.
Je, kama T.I atatekeleza mpango wake wa kustaafu kweli, utamkumbuka zaidi kupitia wimbo upi? 🎤🔥


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni