Breaking


Jumatano, 4 Februari 2026

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI BORA YA ARDHI KULINDA HIFADHI NA MAZINGIRA

 


Serikali imewataka wananchi kuzingatia kikamilifu mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha mahitaji ya sasa na ya baadaye katika shughuli za kilimo, ufugaji na makazi yanakidhiwa bila kuathiri mazingira na maeneo yaliyohifadhiwa. Hatua hiyo inalenga kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa kikao cha saba cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Chande alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo husika, Mheshimiwa Onesmo Merdson Mnkondya (Mb), aliyehoji mpango wa Serikali kuhusu uwezekano wa kuwapatia wananchi vipande vya ardhi vinavyopakana na Hifadhi Ndogo ya Msitu wa Isalalo inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).


Akifafanua suala hilo, Mhe. Chande amesema Hifadhi ya Msitu wa Isalalo ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai ikiwemo mimea na wanyama, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Amesema msitu huo umezungukwa na vijiji vitano ambavyo ni Itentula, Hamwelo, Nambizo, Ipapa na Utambalila, ambavyo vina mchango mkubwa katika kulinda na kuhifadhi mazingira yanayozunguka hifadhi hiyo.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa Serikali kwa sasa haina mpango wa kugawa au kumega hifadhi hiyo kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu, kwani kufanya hivyo kutahatarisha malengo ya uhifadhi yaliyokusudiwa.


“Hata hivyo, Serikali inaruhusu wananchi kuendesha shughuli ambazo hazikinzani na uhifadhi ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo ufugaji wa nyuki. Baadhi ya wananchi tayari wameanza kunufaika na shughuli hizo ambazo zinakwenda sambamba na malengo ya kulinda mazingira,” amesema Mhe. Chande.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi waliopo maeneo yanayozunguka hifadhi ili kuhakikisha uhifadhi wa misitu unaendelea huku wananchi wakinufaika kiuchumi kupitia shughuli rafiki kwa mazingira.


Hakuna maoni: