Breaking


Jumatatu, 9 Februari 2026

MAHAKAMA YA HONG KONG YAMHUKUMU JIMMY LAI MIAKA 20 JELA, ULIMWENGU WAPAZA SAUTI KUHUSU UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

 


Mahakama ya Hong Kong imemhukumu mfanyabiashara wa vyombo vya habari na mwanaharakati wa demokrasia, Jimmy Lai, kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kushirikiana na mataifa ya kigeni pamoja na kuchapisha machapisho ya uchochezi, makosa yaliyoshtakiwa chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa iliyowekwa na Serikali ya China.


Kwa mujibu wa majaji, adhabu hiyo imetokana na uzito wa makosa aliyotenda, huku wakieleza kuwa sehemu ya kifungo hicho itahesabiwa sambamba na kifungo ambacho Lai alikuwa tayari anakitumikia. Hivyo basi, mfanyabiashara huyo atatumikia jumla ya miaka 18 zaidi gerezani, akiwa tayari ameshikiliwa tangu mwaka 2020.


Jimmy Lai, mwenye umri wa miaka 78 na mwanzilishi wa gazeti maarufu la Apple Daily ambalo sasa limefungwa, alionekana kutabasamu na kuwapungia mkono wafuasi wake alipowasili mahakamani. Tukio hilo liliwapa matumaini baadhi ya wafuasi wake, lakini hali ilibadilika alipoondoka ukumbini, ambapo hisia za huzuni zilishuhudiwa na baadhi ya waliokuwepo kuonekana wakilia.


Hukumu hiyo imeibua ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa, huku viongozi wa dunia na mashirika ya kutetea haki za binadamu wakieleza wasiwasi wao, wakidai kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuendelea kudorora kwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini Hong Kong.


Wadadisi wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu wanasema kesi ya Jimmy Lai ni mfano wa mwelekeo mpya wa utekelezaji wa sheria za usalama wa taifa, unaoathiri moja kwa moja wanahabari na wanaharakati wa demokrasia katika eneo hilo.


Hakuna maoni: