Mashabiki wa bingwa wa dunia mara saba wa mbio za Formula One (F1), Lewis Hamilton, wameonyesha kutoridhishwa na tetesi za mahusiano yake na Kim Kardashian, mpenzi wa zamani wa rapa Kanye West, wakidai kuwa hakuna jambo jema linalotokana na kuwa karibu na familia ya Kardashian.
Mjadala huo mkali umeibuka mitandaoni kufuatia Lewis Hamilton na Kim Kardashian kuonekana pamoja katika mchezo wa fainali ya Super Bowl, ambapo walinaswa wakipeana busu la kimahaba, jambo lililochochea hisia mseto miongoni mwa mashabiki.
Kupitia mitandao ya kijamii, baadhi ya mashabiki wa Hamilton wameeleza wasiwasi wao wakidai kuwa, kwa historia, wanaume waliowahi kuwa katika mahusiano na Kim Kardashian hawajapata maisha ya utulivu baada ya kuachana naye. Wengine wameenda mbali zaidi wakisema kuwa uhusiano huo unaweza kuathiri umakini na mafanikio ya Hamilton ndani na nje ya ulingo wa mashindano.
Hata hivyo, hadi sasa, Lewis Hamilton wala Kim Kardashian hawajatoa tamko rasmi kuthibitisha au kukanusha mahusiano yao, huku tukio la Super Bowl likiendelea kuwa chanzo kikuu cha tetesi hizo.
Lewis Hamilton anaendelea kutambuliwa kama mmoja wa madereva bora zaidi katika historia ya Formula One, akiwa na mataji saba ya dunia, na mashabiki wake wengi wakitamani aendelee kulinda rekodi na hadhi yake ndani ya mchezo huo maarufu duniani.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni