Breaking


Jumatano, 11 Februari 2026

“MKOSI WA DRAKE” WAENDELEA: APOTEZA TSH BILIONI 2.59 SUPER BOWL AKIWA ANASUBIRI KUACHIA ‘ICEMAN’



Rapa maarufu duniani, Drake, ambaye kwa sasa anajiandaa kuachia albamu yake mpya “Iceman”, ameendelea kugonga vichwa vya habari – safari hii si kwa muziki, bali kwa mikeka yake ya mamilioni inayozidi kubuma.


Katika fainali ya Super Bowl 2026 iliyowakutanisha New England Patriots dhidi ya Seattle Seahawks, Drake aliamua kujaribu bahati yake kama ilivyo kawaida yake. Bila kusita, aliweka dau la Dola za Marekani milioni 1 (takribani Tsh Bilioni 2.59) akibashiri kuwa Patriots wangebeba taji.

Kinachofanya dau hili livutie zaidi ni kwamba timu aliyoiwekea mkeka, Patriots, inachezewa na Stefon Diggs  baba mtoto wa rapa Cardi B.


Mashabiki Walimwonya, Hakusikiliza

Kabla ya mchezo kuanza, Drake alishiriki slip ya dau lake kwa wafuasi wake zaidi ya milioni 141 kwenye Instagram. Mashabiki wengi walimshauri abadili msimamo wake na kuweka dau kwa Seahawks, wakidai “mkosi wake wa kamari” ungeendelea.


Hata hivyo, Drake aling’ang’ania msimamo wake kuwa Patriots wangeshinda.


Matokeo Yakamgeuka

Dakika 90 zilipomalizika, mambo hayakuwa kama alivyotarajia. Patriots walichapwa kwa alama 29-13, na hivyo Drake kupoteza rasmi dau lake la mamilioni.


Hii imeongeza mjadala mtandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimkosoa kwa kile wanachokiita “uraibu wa kamari”, wakati wengine wakichukulia hali hiyo kama sehemu ya burudani yake binafsi.


Rekodi Isiyovutia

Kwa mujibu wa ripoti maalum, Drake amepoteza mara 30 kati ya mikeka 54 aliyowahi kucheza – takwimu zinazoendeleza simulizi ya “Drake Curse” maarufu mitandaoni.

Hata hivyo, hasara hizo hazijaonekana kumkatisha tamaa. Katika mahojiano aliyoyashiriki kupitia Instagram, Drake alikiri kwa utani kuwa anaonekana kuwa na “mkosi sana linapokuja suala la mikeka yangu kubuma kila wakati.”

Wakati mashabiki wakisubiri kuona kama atavunja laana hiyo siku zijazo, macho mengi kwa sasa yako kwenye uzinduzi wa albamu yake mpya “Iceman” je, muziki wake utaondoa presha ya mikeka?


Endelea kufuatilia kwa taarifa zaidi.


Hakuna maoni: