Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), leo Februari 11, 2026 amezindua na kukabidhi rasmi miundombinu 21 ya utalii iliyojengwa katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha, Mikumi pamoja na Msitu wa Mazingira Asilia wa Kilombero.
Miradi hiyo imegharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 114.62, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Miundombinu hiyo inatarajiwa kuongeza ubora wa huduma na vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, ambao umeendelea kuwa kitovu muhimu cha maliasili na hifadhi za kipekee barani Afrika. Aidha, uwekezaji huo utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maliasili na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za utalii.
Mbali na kukuza sekta hiyo, miradi hiyo pia inalenga kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hizo, ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia shughuli mbalimbali za utalii.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali katika kuendeleza utalii endelevu, huku ikiimarisha ustawi wa jamii na kuhifadhi rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni