Breaking


Jumamosi, 7 Februari 2026

MUSEVENI AWASILI TANZANIA: MAZUNGUMZO YA NISHATI NA USHIRIKIANO WA KIKANDA YAWEKA HISTORIA MPYA



Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amewasili nchini Tanzania leo kwa ziara ya kikazi ya siku moja, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili jirani.


Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Rais Museveni alipokelewa na Waziri asiye na Wizara Maalum, Profesa Paramagamba Kabudi, kabla ya kuelekea Ikulu kwa ajili ya mazungumzo rasmi.


Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Museveni amepokelewa na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo viongozi hao wawili wanafanya mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, na kuimarisha mshikamano wa kikanda.

Miongoni mwa ajenda kuu zinazojadiliwa ni sekta ya nishati, hususan Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), unaotarajiwa kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania, Uganda, na ukanda mzima wa Afrika Mashariki kupitia ajira, mapato ya serikali, na ukuaji wa miundombinu.


Kwa ujumla, ziara hii inaakisi dhamira ya nchi hizo mbili kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, usalama, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kuimarisha amani na ustawi wa kikanda.

Aidha, hii ni ziara ya kwanza kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupokea kiongozi wa nchi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na pia ni safari ya kwanza ya nje kwa Rais Museveni tangu aapishwe kuendelea na uongozi baada ya uchaguzi wa mwaka huu ikiipa ziara hii uzito wa kihistoria na kisiasa.

 

Hakuna maoni: