Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa SIngapore nchini tanzania mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Balozi Douglas Foo mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 25 Februari, 2026 katika Ofisi ndogo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dar es salaam.
Miongoni mwa masuala mbalimbali waliyozungumza ni pamoja na ushirikiano ikiwemo umuhimu wa Tanzania kusaini na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Upatanishi maarufu kama Singapore Convention on Mediation, Sheria za kijiditali na Akili mnemba na namna ya kuanzisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Singapore.
Katika mazungumzo yao pande zote zimeonesha umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili kuwawezesha kuendana na maendeleo ya uchumi, uwekezaji, biashara na teknolojia Duniani.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemshukuru Balozi Foo kwa kutembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mara nyingine tena baada ya ziara yake ya mwaka jana.
Katika hatua nyingine, Mhe. Johari ameeleza kwa kina kwamba kadri Uwekezaji na Biashara unavyozidi kukua migogoro pia haiepukiki hivyo ni muhimu kuanza kufikiria njia mbadala za utatuzi wa migogoro ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi mahakamani.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kwamba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo tayari kuendelea kujifunza njia mbalimbali za utatuzi wa migogoro ikiwemo njia ya upatanishi katika *Singapore Convention on Mediation.*
Kwa upande wake, Balozi Foo ameeleza kuwa Singapore ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika mageuzi ya sheria kwa kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ambayo Singapore imepiga hatua ikiwemo sheria za kijiditali, ulinzi wa taarifa binafsi, na mapambano dhidi ya rushwa.
Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kutengeneza mpango kazi utakaoweka njia ya ushirikiano na utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni