Breaking


Alhamisi, 26 Februari 2026

TASAC YASHIRIKI MKUTANO WA KIKANDA WA USALAMA WA BAHARINI BAHARI YA HINDI NA PASIFIKI


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeshiriki Mkutano wa Kikanda wa Usalama wa Baharini wa eneo la Bahari ya Hindi na Bahari ya Pasifiki, mkutano uliowaleta pamoja wadau wa usalama majini eneo la Bahari ya Hindi Kusini mwa Afrika na eneo la Indo Pacific kujadili kwa kina hali ya usalama, changamoto zinazoikabili sekta hiyo, na mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.


Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri Majini pamoja na Meneja Usalama na Utunzaji Mazingira Majini TASAC, Nahodha Alex Katama.


Katika mkutano huo, wajumbe walibadilishana uzoefu kuhusu vitisho vinavyoathiri usalama wa baharini, ikiwemo uharamia, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya dawa za kulevya, na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa vyombo vya majini.


Katika kuendeleza ushirikiano wa kiufundi, ujumbe wa TASAC pia ulitembelea Jeshi la Wanamaji la Réunion, ambako walifanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano. 


Majadiliano yalijikita katika mafunzo ya pamoja, kubadilishana utaalamu, na matumizi ya mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa vyombo vya majini kwa lengo la kuzuia na kudhibiti uhalifu wa mipakani, hususan usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya.


Aidha, suala la kujenga na kuimarisha uwezo wa wafanyakazi wa Kituo cha Uratibu wa shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MRCC) lilijadiliwa, likilenga kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za uokoaji na usalama baharini. 


Ushirikiano huu unatarajiwa kuimarisha zaidi uwezo wa kitaifa na kikanda katika kukabiliana na changamoto za usalama wa usafiri majini na kulinda maslahi ya kiusalama katika Bahari ya Hindi na Pasifiki.

Hakuna maoni: