Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), utakaofanyika Oktoba 6 hadi 9, 2026 jijini Dar es Salaam, ukilenga kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira ya bahari na pwani.
Akizungumza Dodoma, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, alisema serikali imeunda kamati ya kitaifa kuratibu maandalizi ya mkutano huo ili kuhakikisha unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Alieleza kuwa Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Nairobi unaohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira ya bahari ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi, huku mikutano ya wanachama ikifanyika kila baada ya miaka miwili.
Katika mkutano wa 11 uliofanyika mwaka 2024 nchini Madagascar, Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano wa 12 unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Sambamba na hilo, Tanzania pia itashiriki Kongamano la 11 la Kimataifa la “Our Ocean Conference” litakalofanyika Juni 2026 jijini Mombasa, Kenya.
Mkurugenzi wa Uchumi wa Buluu, Bi. Magdalena Ngotolainyo, alisema mkutano huo utahusisha zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa mikutano hiyo itafungua fursa za uwekezaji katika uchumi wa buluu, pamoja na kuimarisha sekta za uvuvi na utalii.
Kwa upande wake, Mhandisi Gregory Mella alisema mkutano huo utasaidia kulinda rasilimali za bahari na kuhakikisha wananchi wananufaika nazo kwa njia endelevu.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni