Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki uzinduzi wa mpango wa “Go Green With Imbeju Youth Cohort 2026” iliyoandaliwa na CRDB Bank Foundation, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
Uzinduzi huo uliwakutanisha zaidi ya vijana na wanawake 2,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kushiriki katika shughuli za uchumi wa kijani.
Ushiriki wa NEMC katika mpango huo ni kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wezeshi kwa vijana, huku nguzo yake ya tatu ikiweka msisitizo mkubwa katika masuala ya usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia mpango huo, vijana wanahamasishwa kushiriki katika kilimo cha kisasa, ubunifu wa teknolojia rafiki kwa mazingira na miradi ya ujasiriamali inayozingatia misingi ya Uhifadhi na Usimamizi endelevu wa rasilimali.
Ushiriki wa NEMC umeleta tija kwa kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa chini ya mpango huo inazingatia Sheria na Kanuni za mazingira nchini. Kama Taasisi yenye dhamana ya kusimamia na kuhifadhi mazingira, NEMC itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na miongozo itakayowawezesha vijana kuchangia ukuaji wa uchumi huku wakilinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni