Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika mchakato wa utungaji na uhuishaji wa Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa, akisema hatua hiyo itasaidia kuwajengea wananchi uelewa wa sheria hizo na kurahisisha utekelezaji wake katika maeneo yao.
Mheshimiwa Paresso ametoa kauli hiyo leo Februari 10, 2026 jijini Dodoma, wakati akiongoza kikao cha mafunzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Sheria tatu za Mamlaka za Serikali za Mitaa na uhusiano wake na Sheria Ndogo zinazotungwa na mamlaka hizo.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Paresso pamoja na wajumbe wa kamati hiyo waliishauri Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kufanya mapitio ya Sheria Ndogo ambazo zimepitwa na wakati, kwa lengo la kuzihuisha au kuziondoa kabisa pale zitakapobainika kutotekelezeka au kutokidhi mahitaji ya sasa ya jamii.
Akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mheshimiwa Profesa Riziki Shemdoe, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Kaspar Mmuya, amesema TAMISEMI itazingatia maelekezo ya kamati kwa kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu wakati wa utungaji wa Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatua itakayoongeza uelewa na kuimarisha utekelezaji wake.
Aidha, Mheshimiwa Mmuya ameihakikishia kamati hiyo kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI itafanya mapitio ya Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kujiridhisha kama zinaendana na wakati uliopo, na kusisitiza kuwa sheria zitakazobainika kupitwa na wakati zitahuishwa au kuondolewa.
Katika kikao kazi hicho cha mafunzo, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo walipata fursa ya kupitia Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287 pamoja na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kwa lengo la kuongeza uelewa na ufanisi katika kusimamia Sheria Ndogo nchini.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni