Ndege ya raia iliyokuwa imewabeba abiria 50 na wafanyakazi 5 imelazimika kutua baharini karibu na ufuo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde, Mogadishu, kufuatia hitilafu ya kiufundi iliyojitokeza muda mfupi baada ya kupaa. Tukio hilo limetamatika salama baada ya watu wote 55 kuokolewa bila majeraha makubwa.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia, ndege hiyo ilikuwa imepangwa kusafiri kutoka Mogadishu kuelekea Galkayo, mji mkuu wa mkoa wa Mudug, kabla ya marubani kuripoti tatizo la kiufundi na kuomba kurejea uwanjani.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Ahmed Macalin Hassan alisema kuwa ndege ilifanikiwa kutua lakini haikuweza kusimama kwenye barabara ya kurukia na kutua, hali iliyomlazimu rubani kuielekeza hadi eneo la bahari karibu na uwanja wa ndege.
Vikosi vya uokoaji vilifika eneo la tukio haraka, na kufanikisha kuwahisha abiria na wafanyakazi wote hadi sehemu salama. Hakuna vifo wala majeraha makubwa yaliyoripotiwa.
Kwa upande wake, Shirika la Ndege la Starsky limethibitisha kuanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha hitilafu hiyo, huku likimpongeza rubani kwa uamuzi wa kijasiri na wa kitaalamu uliosaidia kuokoa maisha ya wote waliokuwa ndani ya ndege.
Maafisa wa usafiri wa anga wamesema uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu halisi ya tukio hilo na kutathmini athari zozote kwa usalama wa safari za anga siku zijazo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni