Breaking


Jumanne, 3 Februari 2026

SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI YA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI KATIKA MAKAZI YA WANANCHI

 


Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya askari wa wanyamapori pamoja na matumizi ya ndege nyuki (drones) ili kuimarisha doria katika makazi ya wananchi na maeneo ya hifadhi, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wanaovamia makazi ya watu.


Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa kikao cha 6 cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipokuwa akijibu swali la Mhe. Cecilia Daniel Paresso (Mb). Swali hilo lilitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu wanaotoka katika Hifadhi ya Ngorongoro na Ziwa Manyara na kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Akijibu swali hilo, Mhe. Chande ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Askari wa Wanyamapori katika Kijiji cha Lostete kilichopo mpakani mwa hifadhi. Aidha, Serikali inatumia Askari wa Vijiji (VGS) wanaoshirikiana kwa karibu na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi.


Katika hatua nyingine, Mhe. Chande amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali inatarajia kujenga uzio wa umeme wenye urefu wa kilometa 15, ambao unalenga kuzuia tembo na wanyamapori wengine kuingia kwenye maeneo ya makazi ya wananchi na kusababisha madhara.

“Serikali imeandaa Mkakati Mpya wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa miaka kumi kuanzia 2025/26 hadi 2035/36. Mkakati huu utatekelezwa kwa ushirikiano wa wizara za kisekta ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” ameeleza Mhe. Chande.


Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkakati huo unalenga kuhakikisha juhudi za kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori zinafanyika kwa pamoja, kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi pamoja na uhifadhi wa rasilimali za taifa.


Hakuna maoni: