Wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wamekutana Jijini Dodoma kujadili utabiri wa msimu wa Masika 2026 na kutoa ushauri wa kisekta, katika Mkutano wa 25 wa Wadau wa Sekta ya Hali ya Hewa uliofanyika tarehe 2 Februari 2026.
Mkutano huo ni sehemu ya mkakati endelevu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa kuwashirikisha wadau katika utoaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mheshimiwa Jaji Mshibe Ali Bakari, alisema msimu wa Vuli wa mwaka 2025 ulitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, huku usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kufikia asilimia 94.1, kiwango alichokitaja kuwa cha juu sana.
“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kuiamini TMA, kuzingatia taarifa zinazotolewa na kuzitumia ipasavyo katika shughuli zao za kila siku,” alisema Mh. Jaji Bakari.
Aidha, alisisitiza kuwa majadiliano ya mvua za Masika 2026 yazingatie kwa kina athari zinazoweza kujitokeza, pamoja na kutoa ushauri wa hatua stahiki kwa ajili ya matumizi ya taarifa hizo katika sekta mbalimbali zinazochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Changa, alisema Mamlaka imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza pengo la uelewa wa tahadhari za hali ya hewa kwa kushirikisha wadau katika uandaaji wa taarifa sahihi na zenye tija.
Dkt. Changa aliongeza kuwa TMA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, hali iliyoiwezesha Tanzania kutambuliwa kama moja ya nchi zinazoaminika katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa duniani. Kutokana na mafanikio hayo, Tanzania imechaguliwa kuandaa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wataalam Bingwa wa Hali ya Hewa Duniani, unaotarajiwa kufanyika Juni 2026.
Kwa upande wao, wadau walitoa pongezi kwa TMA kwa kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii. Akizungumza kwa niaba ya wadau, Kaimu Mkurugenzi wa Kamisheni ya Maafa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ndg. Muhidin Ali Muhidin, alisema taarifa za hali ya hewa ni nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kulinda usalama wa wananchi na mali zao.
TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa Masika 2026 tarehe 5 Februari 2026, ambao unatarajiwa kuwa mwongozo muhimu kwa sekta mbalimbali nchini.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni