Mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili B (HEP 2B) unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi katika Mkoa wa Katavi kwa kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji, pamoja na kukuza uwekezaji na ajira kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo, Februari 6, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoto, mara baada ya kutambulishwa kwa mkandarasi Kampuni ya M/s ETDCO Ltd atakayetekeleza mradi wa HEP 2B wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 358, vitakavyonufaisha wakazi zaidi ya 11,536 mkoani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, RC Mrindoto amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika utawezesha wananchi kuacha kuuza mazao ghafi na badala yake kuyachakata ili kuongeza thamani na kipato.
“Badala ya kuuza malighafi, tutaanza kuuza bidhaa zilizochakatwa. Umeme utapandisha thamani ya mazao yetu kwa kuwa yatachakatwa katika mazingira bora,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo utachangia kukuza uchumi wa mkoa kwa kuvutia uwekezaji, kuanzisha viwanda vidogo na vya kati, na kufungua ajira kwa vijana, wanawake, wazee na makundi mbalimbali ya kijamii.
RC Mrindoto amemuelekeza mkandarasi kuanza kazi mara moja kwa kasi na ufanisi, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji matokeo halisi.
“Wananchi wanahitaji umeme, si maneno, si ahadi, wala ratiba zisizotekelezeka. Kazi ianze kwa kasi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mussa Muze, amesema lengo kuu la mradi wa HEP 2B ni kuongeza upatikanaji wa umeme katika vitongoji vya Katavi na kuchochea maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi.
Naye, Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Katavi, Gilbert Furia, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi na kutumia fursa ya umeme kujiinua kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji na biashara.
Kwa upande wa mkandarasi, Abdalah Mitenda kutoka Kampuni ya M/s ETDCO Ltd amemhakikishia RC Mrindoto kuwa utekelezaji wa mradi utazingatia ushiriki wa wananchi kwa kuwapa kipaumbele wakazi wa maeneo husika katika shughuli zitakazofanyika, huku akiwahimiza kuchangamkia fursa zitakazojitokeza.
Mradi wa HEP 2B unatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu itakayobadilisha maisha ya wananchi wa Katavi kwa kuleta nishati ya uhakika na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi mkoani humo.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni