Familia ya soka nchini Kenya ipo katika majonzi mazito kufuatia kifo cha beki wa klabu ya Kakamega Homeboyz FC, Silas Abungana, aliyefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na uongozi wa Kakamega Homeboyz, Abungana alifariki dunia dakika chache kabla ya saa sita usiku wa kuamkia Jumatano, Februari 4, 2026, baada ya hali yake ya afya kuzorota licha ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake.
Taarifa zinaeleza kuwa beki huyo alipata majeraha makubwa ya kichwa kufuatia shambulio lililotokea usiku wa Jumanne, Februari 3, 2026, muda mfupi baada ya kurejea nyumbani akitokea kwenye majukumu yake ya kikazi. Tukio hilo linadaiwa kuhusisha mgogoro wa kifamilia, ambapo mdogo wake anatajwa kuhusika, kufuatia mvutano uliodumu kwa muda mrefu ndani ya familia.
Chanzo cha mvutano huo kinaelezwa kuwa ni masuala ya ndoa, ambapo baadhi ya ndugu wa marehemu walikuwa wakimsukuma aachane na mke wake wakidai kuwa hafai kwa familia. Mzozo huo ulidaiwa kuchochea ugomvi uliosababisha majeraha yaliyompelekea kulazwa hospitalini, kabla ya kufariki dunia.
Kifo cha Silas Abungana kimeacha pengo kubwa katika klabu ya Kakamega Homeboyz, mashabiki wa soka, pamoja na familia na marafiki waliomfahamu kama mchezaji mwenye nidhamu, kujituma na mchango mkubwa ndani na nje ya uwanja.
Uongozi wa klabu, Shirikisho la Soka nchini Kenya, pamoja na wadau mbalimbali wa michezo wameendelea kutoa salamu za rambirambi, wakilitaka tukio hilo lichunguzwe kwa kina ili haki itendeke.
Abungana anakumbukwa kama mmoja wa mabeki waliokuwa wakikua kwa kasi katika Ligi Kuu ya Kenya, na kifo chake ni pigo kubwa kwa maendeleo ya soka la nchi hiyo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni