Familia ya rapa na mtayarishaji mashuhuri wa muziki wa hip hop, Lil Jon, imo katika hali ya taharuki kufuatia taarifa za kupotea kwa mtoto wake, Nathan Smith, anayejulikana pia kwa jina la kisanii DJ Young Slade, katika jimbo la Georgia, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Milton Police Department, Nathan Smith mwenye umri wa miaka 27 alionekana kwa mara ya mwisho Februari 3, majira ya saa 12 asubuhi. Polisi wamesema kuwa Nathan aliondoka nyumbani kwake kwa miguu, bila kuwa na simu ya mkononi, hali inayoongeza wasiwasi juu ya usalama wake.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa huenda Nathan alikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa wakati anaondoka nyumbani, na mamlaka zinaamini kuwa anahitaji msaada wa haraka. Kutokana na hali hiyo, polisi wamewaomba wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa yoyote itakayosaidia kumtambua au kumpata.
Familia na marafiki wa karibu wameeleza kuwa wana hofu kubwa juu ya usalama wa Nathan, wakisisitiza kuwa tukio hilo limewaacha katika mshtuko mkubwa. Nathan anaelezwa kuwa na macho ya kahawia, nywele fupi nyeusi, na ana urefu wa futi 5 na inchi 9.
Baba yake, Lil Jon (jina halisi Jonathan Smith), ni msanii mwenye ushawishi mkubwa katika muziki wa hip hop duniani, sambamba na kuonekana kwenye vipindi mbalimbali vya televisheni ikiwemo The Apprentice, Bachelor in Paradise, pamoja na kipindi chake cha HGTV kiitwacho Lil Jon Wants to Do What?.
Akifuata nyayo za baba yake katika tasnia ya burudani, DJ Young Slade amewahi kujitokeza kama DJ kwenye kipindi cha BET Looped In Live, filamu Battlefield America, na pia kipindi cha MTV Family Legacy, ambacho huangazia watoto wa mastaa wakisimulia safari zao.
Mpaka sasa, jitihada za kumtafuta zinaendelea, huku jamii ikihimizwa kutoa msaada wowote unaoweza kusaidia kupatikana kwake salama.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni