Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam mnamo Februari 8, 2026, baada ya kukamilika kwa ukarabati mkubwa uliotokana na tukio la moto pamoja na ujenzi wa soko jipya la kisasa.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema kuwa Soko la Kariakoo kwa sasa limekamilika kwa asilimia 100, huku zaidi ya Shilingi bilioni 28 zikitumika kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na kujenga soko jipya linalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wa kisasa.
Mhe. Chalamila ameeleza kuwa soko hilo sasa lina zaidi ya vizimba 1,500, ambavyo vitawapa wafanyabiashara mazingira salama, ya kisasa na rafiki kwa kufanya shughuli zao za kiuchumi. Ameongeza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha masoko ya kimkakati nchini na kukuza uchumi wa wananchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam, hususan wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo muhimu, ili kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kushuhudia tukio la kihistoria linalotarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chalamila ametoa agizo kwa wafanyabiashara wadogo waliokuwa wamefunga barabara za kuingia katika Soko la Kariakoo kuhakikisha wanaondoa vizuizi hivyo kabla ya Februari 8, 2026. Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuruhusu upatikanaji wa soko kwa urahisi, kudhibiti usalama na kuhakikisha uzinduzi unafanyika kwa utulivu na mpangilio mzuri.
Uzinduzi wa Soko la Kariakoo unatarajiwa kuwa hatua mpya katika kuimarisha biashara, ajira na maendeleo ya kiuchumi, huku soko hilo likirejea rasmi kama moyo wa biashara kwa maelfu ya wafanyabiashara na wateja kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni