Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka Wahandisi wa Mikoa na Wasimamizi wa Miradi ya Umwagiliaji nchini kuzingatia uzalendo wa hali ya juu na kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali unaleta matokeo chanya na tija iliyokusudiwa kwa wananchi.
Akizungumza mkoani Iringa wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Kheri James alisema ufanisi wa miradi ya umwagiliaji unategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu, uadilifu na usimamizi thabiti wa wataalamu wanaohusika moja kwa moja na utekelezaji wa miradi hiyo. Mafunzo hayo yalihusu Usimamizi wa Mikataba, Sheria za Ununuzi, Uhandisi wa Geoteknolojia (Utafiti wa Miamba) pamoja na kubadilishana uzoefu miongoni mwa washiriki.
Mkuu huyo wa Mkoa alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa miongozo na fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya umwagiliaji, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni nguzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo.
Aidha, Kheri James aliipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Raymond Mndolwa, kwa kuimarisha weledi kazini na kudhibiti migogoro mbalimbali inayokwamisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Aliongeza kuwa msimamo wa kusimamia viwango na taaluma ndiyo unaohakikisha miradi mikubwa, ikiwemo ile ya mabilioni ya shilingi kama Mradi wa Mkombozi, inaleta matokeo halisi badala ya kubaki kwenye makaratasi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, alisema Tume imejipanga kusimamia miradi ya umwagiliaji kwa karibu zaidi ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa gharama zilizopangwa, hatimaye kuwanufaisha wakulima na taifa kwa ujumla.
Mndolwa alibainisha kuwa NIRC inaendelea na ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji, shughuli za uvunaji na uhifadhi wa maji, pamoja na utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira. Alisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya uzalendo wa kulinda rasilimali za Taifa, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao, kujitosheleza kwa chakula cha ndani na hatimaye kuchangia katika kuilisha duni





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni