Breaking


Ijumaa, 6 Februari 2026

WAFANYABIASHARA KARIAKOO WAKUBALI MFUMO MPYA WA IDRAS, WAJIANDAA KUANZA RASMI FEBRUARI 9




Wafanyabiashara nchini, hususan wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wameukubali rasmi Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) huku wakitangaza utayari wao wa kuanza kuutumia kuanzia Jumatatu, Februari 9, 2026.

Akizungumza leo Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Bw. Severin Mushi, amesema wafanyabiashara wako tayari kuanza safari mpya ya matumizi ya IDRAS kwa ushirikiano wa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Bw. Mushi amesema mafunzo yaliyotolewa na TRA yamekuwa chachu muhimu katika kuwajengea wafanyabiashara uelewa na imani juu ya mfumo huo mpya, akieleza kuwa IDRAS inatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika ulipaji wa kodi hapo awali.


“Kupitia mafunzo haya, hofu iliyokuwepo mwanzo imeondoka kwa kiasi kikubwa. Sasa tuna uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kutumia mfumo huu na faida zake kwa mfanyabiashara na Serikali kwa ujumla,” amesema Bw. Mushi.

Ameongeza kuwa ni jambo la kawaida kwa mabadiliko mapya kuleta wasiwasi kwa wanaoyapokea, lakini amesisitiza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia hayaepukiki katika dunia ya sasa. Kwa mujibu wake, wafanyabiashara hawana budi kuendana na mabadiliko hayo ili kuboresha ufanisi wa biashara zao na ulipaji wa kodi.


Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ameomba TRA kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kutatua changamoto ya mtandao katika baadhi ya maeneo ya biashara, hasa Kariakoo, akibainisha kuwa upatikanaji wa mtandao wa uhakika ni nguzo muhimu katika matumizi bora ya mfumo wa IDRAS.

Aidha, Bw. Mushi amewahimiza wafanyabiashara wote kuwa tayari kuupokea mfumo huo na kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na TRA, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha ulipaji wa kodi unakuwa rahisi, wa haraka na wenye tija kwa pande zote.


“Tumejiandaa kuupokea mfumo kuanzia Jumatatu ya tarehe 9 mwezi huu. Kikubwa ni kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha tunalipa kodi na mifumo ya ulipaji inakuwa rafiki kwa mfanyabiashara,” amesema.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo amependekeza kuwepo kwa kipindi cha mpito cha mafunzo kwa wafanyabiashara ili kuwapa muda wa kutosha kuuzoea na kuuelewa mfumo huo mpya kabla ya utekelezaji wake kamili.

“Angalau miezi mitatu ya mwanzo iwe ni ya mafunzo na uelimishaji. Wafanyabiashara wakishauuelewa mfumo vizuri, utekelezaji wake utakuwa rahisi na wenye ufanisi zaidi,” amesisitiza Bw. Mushi.

Hatua hii inaonesha dhamira ya wafanyabiashara kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, huku IDRAS ikitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi chanya katika usimamizi wa kodi nchini.

 

Hakuna maoni: