Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo, Norway katika Ukanda wa Africa (IDN- AFRICA) kupitia Mradi wa Uoteshaji wa Malisho ya Mifugo na Ustahimilivu wa Tabianchi (J- CRISD) imeanza kutoa mafunzo kwa wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuzalisha malisho aina ya Juncao ili kukabiliana na uhaba wa malisho na kuwa na ufugaji wenye tija.
Mafunzo hayo ambayo yameanza Februari 18, 2026 yameshirikisha wafugaji na wataalamu wa mifugo kutoka kata za Mpwayungu, Itiso, Mvumi, Makang’wa na Chilonwa ambapo lengo ni kutoa mafunzo kwa vitendo moja kwa moja kwenye maeneo ya wafugaji.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino Bi. Zaina Msangi amesema ujio wa mradi huo wa kuhamasisha wafugaji kulima malisho utasaidia kuondoa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
“Kwa upande wetu Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino hatukuwa na elimu hii ya malisho, kwahiyo mradi huu utasaidia kufikisha elimu ya malisho kwa wafugaji na hii itasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji” alisema Bi. Msangi.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Afisa Usimamizi wa Nyanda za Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Boniphace Shija amesema serikali imeamua kuawahamasisha wafugaji kulima malisho ili kukabiliana na uhaba wa malisho nchini.
“ Tumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikitokea kwa wafugaji hasa uwepo wa vifo vingi kipindi cha kiangazi, ndio maana serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi imeamua kuja na mbinu ya kuwahamasisha wafugaji kulima malisho katika mashamba yao binafsi” alisema Bw. Shija.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la IDN Africa Ukanda wa Africa Mashariki, Bw. Jonathan Kifunda amesema mradi huo utarajiwa kuwafikia wafugaji 500 katika halmashauri hiyo kuzalisha malisho ya mifugo kwa kipindi cha miaka miwili, hatua inayolenga kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhama hama.
Kwa upande wake, mfugaji kutoka Itiso Wilayani Chamwino, Bw. Juma Maguu baada ya mafunzo hayo amesema elimu ya kuwabadilisha wafugaji iendelee kutolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuondokana na ufugaji wa mazoea na kuhimiza ulimaji wa malisho



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni