Breaking


Jumatatu, 2 Februari 2026

WAHANDISI WA UMWAGILIAJI WATAKIWA KUFUTA DHANA YA ‘KUKARIRI’ KATIKA USIMAMIZI WA MIRADI – MWELI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amewataka Wahandisi wa Umwagiliaji nchini kuachana na kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kutumia mbinu bunifu na uzoefu wa kitaalamu katika kusimamia miradi ya umwagiliaji, ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa Taifa. 

Akifungua mafunzo ya usimamizi wa mikataba, sheria za ununuzi na utafiti wa miamba katika mabwawa mkoani Iringa, Mweli aliwataka wahandisi kufuta dhana ya kukariri kwa kuwa usimamizi wa wakandarasi unahitaji mbinu za ziada na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wadau wengine. 

Katibu Mkuu amebainisha kuwa mafunzo hayo, yanayofadhiliwa na Serikali kupitia Mradi wa TRIP 2 kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, yanalenga kuwajengea uwezo wahandisi kufanya maamuzi sahihi katika hatua za usanifu na ujenzi ili kupunguza athari na kuboresha ubora wa miradi. 

Aidha, Mweli alisisitiza umuhimu wa watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua taarifa za upembuzi yakinifu na kusimamia washauri waelekezi kwa umakini zaidi, ili miradi iwe na thamani ya fedha na kuleta matokeo makubwa. 

Katika ziara yake mkoani Iringa, Mweli ametembelea Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 56 na kuipongeza Tume kwa kukamilisha mradi huo wa kimkakati, ambao tayari umeanza kunufaisha wakulima upande wa mashariki wa skimu hiyo. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amewataka wahandisi wa mikoa kusimamia kwa nidhamu miradi mikubwa 146 inayotekelezwa na Tume, akisisitiza umuhimu wa uelewa wa sheria za ununuzi, usimamizi wa mikataba na makusanyo ya mapato ya ndani. 

Aidha, Mndolwa amewataka watendaji kuzingatia suala la makusanyo ya mapato ya ndani, akieleza kuwa ni lazima kila mhandisi wa mkoa ahakikishe skimu zinalipa tozo. 

Viongozi hao pia wamehimiza wahandisi kushirikisha wananchi tangu hatua za awali za usanifu wa miradi ili kuepusha migogoro ya fidia, wakibainisha kuwa miradi ya Tume haina utaratibu wa kulipa fidia bali inahitaji ushirikishwaji wa jamii.

Hakuna maoni: