Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amezitaka taasisi zote zinazotekeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kutumia kikamilifu maeneo yao makubwa ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa malisho ya mifugo, hatua itakayosaidia kuimarisha ufugaji wa kibiashara nchini.
Waziri Bashiru ametoa kauli hiyo Januari 31, 2026, wakati wa ziara yake ya ukaguzi katika Kituo cha BBT cha unenepeshaji wa mbuzi na kondoo kilichopo Kongwa, mkoani Dodoma. Katika ziara hiyo, amezitaka taasisi za umma zikiwemo Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa malisho kwa njia ya kibiashara.
Amesema kuwa taasisi hizo zina rasilimali zote muhimu ikiwemo ardhi ya kutosha, wataalam wabobezi pamoja na uzoefu mkubwa, hivyo zina uwezo wa kuwa vinara katika uzalishaji wa malisho bora yatakayosaidia kuongeza tija katika sekta ya mifugo.
“Vituo vyetu vyote vyenye ardhi kubwa kama TALIRI, NARCO na LITA, kwa kuwa tuna utaalam na uzoefu wa kutosha, nguvu zote zielekezwe kwenye uzalishaji wa malisho. Mimi ningefurahi kuona kituo hiki kikijikita zaidi kama BBT ya malisho,” alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha, Waziri huyo amehimiza wafugaji nchini kupewa elimu ya uzalishaji na matumizi sahihi ya malisho, akisisitiza kuwa hatua hiyo itapunguza gharama za ufugaji na kuongeza uzalishaji wa mifugo. Pia ameagiza utekelezaji wa programu ya BBT uishirikishe kwa karibu Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia sekta ya mifugo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daudi Mayeji, akitoa taarifa ya utekelezaji wa programu ya BBT amesema wizara hiyo imetengewa dola za Marekani milioni 32.8, sawa na shilingi bilioni 81, kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo. Amesema pia kuwa uwekezaji wa awali wa Kituo cha BBT cha Kongwa umefikia dola milioni 11.82.
Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ilianza mwaka 2018 kupitia TALIRI kwa kushirikiana na PASS Trust Tanzania, ikiwa na lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia mnyororo wa thamani wa mifugo, kuongeza ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni