Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amepokea rasmi hati za utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) bw. Ashraf Hassan katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kupokea hati hizo, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na IOM, hususan katika kukabiliana na changamoto za uhamiaji, biashara haramu ya binadamu, pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zinazohusika na masuala ya uhamiaji nchini.
Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na IOM kuhakikisha shughuli za uhamiaji zinaendeshwa kwa usalama na kwa kufuata utaratibu. “Ushirikiano wetu unalenga kulinda utu wa binadamu, kuimarisha mifumo yetu ya kitaifa, na kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma,” ameeleza Waziri Kombo.
Kwa upande wake, Bw. Hassan ameahidi kuendeleza ushirikiano thabiti na Serikali ya Tanzania, akieleza kuridhishwa na namna Tanzania inavyochukua hatua madhubuti katika kusimamia masuala ya uhamiaji na kulinda haki za wahamiaji.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni