Breaking


Jumatatu, 23 Februari 2026

WAZIRI ULEGA ATANGAZA MILIONI 10 KWA WAHANDISI WABUNIFU

 


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza mkakati kabambe wa kukuza ubunifu wa wahandisi wa ndani kwa kuahidi kuzawadia mawazo ya kibunifu yatakayosaidia kutatua changamoto zinazoikabili nchi.


Akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ulega amesema mpango huo utawahusu wanafunzi wote wa taaluma za uhandisi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, kwa lengo la kuwajengea ari ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.


Amesisitiza kuwa mtazamo wa wizara ni kuibua na kulea kada ya wanafunzi wabunifu watakaotumia taaluma zao kutatua kero za wananchi, badala ya kujikita katika maandishi yasiyoleta suluhisho la moja kwa moja kwa jamii.


Katika mkutano huo ulioandaliwa na Kitivo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET), Waziri Ulega ametangaza zawadi ya shilingi milioni 10 itakayogawanywa kwa washindi watatu watakaowasilisha mawazo bora na yenye tija kwa jamii.


Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Samia Suluhu Hassan tayari imeahidi kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji wa makundi ya vijana na wanawake, na kwamba mpango wa wizara yake ni nyongeza ya jitihada hizo katika kuwawezesha vijana kutumia ubunifu wao kama chachu ya maendeleo.


Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Rose Upor, amempongeza Waziri Ulega kwa kukubali kuzungumza na wanafunzi na kuwapa mwelekeo mpana kuhusu nafasi yao katika ujenzi wa taifa kupitia taaluma za uhandisi.


Hakuna maoni: